For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Maisha bila Ajira (Sehemu ya Kwanza)

 Naishi Dar es Salaam, maisha ni songombingo,
Ndugu namwona sumu, kwa kuwa ana maringo,
Kwani ameza vitamu, mie kanipa mgongo,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Rohoni sina kinyongo, kwa huu wangu mkosi,
Wapo washika vitengo, watwona vikaragosi,
Wako juu kiviwango, ukianza wadadisi,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Ajira nimetafuta, hadi kwenye Makampuni?
Huko kote sijapata, Urasimu ni Kiini,
Mtaani nimesota, ndugu yangu firauni,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Ndugu niishie kweke, kanifanya hausi-boi,
Kutwa kazi zifanyike, napolala niko hoi,
Ghiliba za mke wake, maseng’enyo hakatai,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

 Nashinda ndani ya geti, utadhani mnyampara,
Nazidi kukaza buti, jijini pamenikera,
Ndugu yangu kizingiti, naishi kama tiara,
   Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Jua kali la utosi, nguo zanukia jasho,
Jamaa ana Ukwasi, mifukoni sina posho,
Sina kazi mahsusi, jijini kwangu kitisho,
   Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Lanikumba sokomoko, pakushika sipaoni,
Kuchapo misukosuko, waishi kisultani,
Naomba mabadiliko, hatilii maanani,
   Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Mwenendo wa kinafiki, jamaa Kabarikiwa,
Tabia za kizandiki, zanifanya kuchachawa,
Nilipo hakukaliki, labda kwa majaliwa,
 Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Fedha zaparaganyika, kweli mie hohehahe,
Lakini sijabweteka, natafuta japo shibe,
Mashaka ya utabaka, yamefanya nizurure,
 Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Ndugu anapokuona, atembea chapuchapu,
Adhani utambana, akupe marupurupu,
Akugeuza mtwana, shibe yako chupuchupu,
 Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment