Kutwa nzima mchakavu, mwana wa kusadikika,
Mambo yanayonisibu, ni vitimbi na pilika,
Nataka fikra pevu, nitoke kufikirika,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Juani nachakarika, shughuli kama Roboti
Rohoni naweweseka, kweli huu Usaliti,
Nyumbani wanapofika, zaanzishwas varangati,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Naota mafanikio, kukwepa hii fitina,
Ajira bado uzio, vijana vichwa twakuna,
Uchumi kisingizio, kwa tulowapa dhamana,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Mlezi wangu kumbuka, mkali kama shubiri,
Asubuhi anang’aka, kama mpiga zomari,
Ndugu huyu ni chikaka, asopenda tafakuri,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Matusi ya rejareja, kabwela wanitukana,
Moyoni sina faraja, waamka wamenuna,
Wanitendea vioja, siwezi hata kuguna,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Mezani anikebehi, utadhani masihara,
Kisa sina maslahi, tumbo latia hasara,
Mwenzenu namsitahi, roho yavuta subira,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Nimepatwa masahibu, mithili ya tingatinga,
Naishi kibubu-bubu, nashindwa hata kulonga,
Mwendo huu wa sulubu, mfano wa karandinga,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Ndugu ana mushikeli, laiti ningelijua,
Sina mustakabali, nazidi kudidimia,
Maisha kitendawili, yangu faraja bandia,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Mwenyeji wangu mchumi, sura ya kihafidhina,
Hila zake za kisomi, mpenda kubaniana,
Mwepesi wa kujihami, kashfa kutupiana,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Sudi yangu maridhawa, sitaki malalamiko,
Napewa ahadi hewa, nisifike niendako,
Usiku najadiliwa, hoja hazina mashiko,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
0 comments:
Post a Comment