For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Khanga (Sehemu ya Pili)

Malezi kwetu watoto, we mhusika mkuu,
Kwa upendo motomoto, nasaha hali ya juu,
Maishani ni fukuto, twaishi bila makuu,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.

Khanga mbona wakubana, haki zako zitambue,
Nawe kazini kazana, jua ulivumilie,
Kama ndoa ni ndoana, acha using’ang’anie!
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.

Kwenye pingu za maisha, pingeni kunyanyasika,
Ngumi na fimbo zatosha, msipende sulubika,
Sulubu kukaribisha, na meno yenu kung’oka,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.

Nanyi shirikianeni, kukwepa dharauliwa,
Kidole cha kiganjani, hakiwezi vunja chawa,
Wanaowaona duni, wanafaa kuzomewa,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.

Kataa kuwekwa nyuma, usije sahaulika,
Usitake kuinama, wasije wakakuruka,
Roho mithili ya chuma, izidi kuimarika,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.

Majogoo yamewika, mama-zetu amkeni,
Msipende kubweteka, mbele nanyi simameni,
Bila ya kutetereka, kamateni usukani,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment