Khanga vazi la heshima, limelea weshimiwa,
Ndiyo mbeleko ya mema, kwetu tuliozaliwa,
Kila napokutazama, wafaa kuzwadiwa,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
Hakika nimeamini, khanga wavaao bora,
Tabia zao makini, wa visiwani na bara,
Wafanyie tathmini, kivitendo wanang’ara,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
Khanga hataki uvivu, afanya shughuli nzito,
Atumia zake nguvu, bila hata ya majuto,
Kazi za ukakamavu, kwake zaleta mapato,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
Hakiki maofisini, khanga ndilo vazi hasa,
Tazama wanazuoni, wenye khanga watikisa,
Wachunguze marubani, khanga wavaa kisasa,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
Wapitishao amri, wapo wanavaa khanga,
Wafanya kazi vizuri, na hawapendi ujinga,
Wapo pia wahariri, taifa letu wajenga,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
Ona kipato cha mji, mwenyewe wakitafuta,
Kilimo kwenye vijiji, peke yako unasota,
Wana watakapo uji, wawapa bila kusita,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
Chunguza walo mjini, wanalopata kidogo,
Watangatanga njiani, biashara zao ndogo,
Wauza mboga-majani, bila hata ya maringo,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
Tazama mama ntilie, kutwa nzima yu moshini,
Yapasa wavumilie, japo wachuma juani,
Kipato watupatie, wana twende masomoni,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
Shughuli mnabebeshwa, wasidhani nyie punda,
Mwapaswa kupumzishwa, na mfaidi matunda,
Msizidi kunyanyaswa, huku miaka yaenda,
Tusikubali unyonge, khanga ndilo vazi letu.
0 comments:
Post a Comment