Kuna watu wa ajabu, ukabila hawaachi,
Wavunja utaratibu, japo nao wananchi,
Huu si ustarabu, kama kula nyama mbichi!,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
Ofisi wafanya zao, wamo wa kabila moja,
Hawatojali wenzao, wasio toka pamoja,
Kabila lao chaguo, labda huzue hoja,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
Roho yao ya umimi, inaturudisha nyuma,
Wenzenu hamtizami, hamna hata huruma,
Ni vizuri mjihami, japo bado mnavuma,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
Yupo anayejiweza, mikono yake birika,
Kivipato aongoza, popote aheshimika,
Kuzitoa akiweza, rohoni anung’unika,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
Ninapigwa bumbuwazi, sipendi kuitwa duni,
Wapo wenye ubaguzi, waona wenzao nyani,
Kujishusha hawawezi, waweka wenzao chini,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
Sisi sote binadamu, weupe ama weusi,
Tusiishi kama ndimu, baadhi kuwa mabosi,
Duniani hatudumu, sote twapita kwa kasi,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
Wapo wengi wanatajwa, tabia zao asidi,
Hakika wana magonjwa, waeneza makusudi!
Wenye tamaa waponzwa, wakidhani wafaidi!,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
Tazama yako taswira, rohoni ujikosoe,
Ukiweza kujichora, kwa hekima jipodoe,
Tamka neo busara, kisha macho yakodoe
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
0 comments:
Post a Comment