For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Kioo (Sehemu ya Kwanza)


Nimekaa kwenye ndoo, huku nimekunja ndita,
Navuta yangu droo, kuna kitu natafuta,
Pembeni kuna kioo, ambacho kinanisuta,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

Mwenzenu ninasumbuka, kwa ninachokitazama,
Ninacheka anacheka, nainama ainama,
Gafla nahuzunika, nae ajishika tama,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

Tabia za walimwengu, zinanistajabisha,
Wapo wapenda majungu, na wale wenye kubisha,
Nilidhania wenzangu, roho zao zinatisha,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

Wacheka mkikutana, rohoni ni tofauti,
Kifanikiwa wanuna, wataki upande chati,
Roho zao za supana, milele kukaza nati,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

Kuna wakabaji koo, hulka zao za chatu,
Waua kama minyoo, ingawa sote tu watu,
Juu ngozi ya kondoo, kumbe ndani mbwa mwitu,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.
Roho mnatoboana, kuvichuma vya dunia!
Hata ngozi mwazichuna, bila kuhisi hatia,
Vibaya mwatendeana, na mali kujipatia,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

Jaribu kuwa makini, hepuka kuwa na pupa,
Kuna wapenda madeni, hawapendi kuyaripa,
Wakitia mifukoni, wataanza kukukwepa,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

Zapita siku tisini, watoto wataka ada,
Mdeni haonekani, imekuwa kawaida,
Ameingia mitini, mpaka awapo na shida,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

Wazee mwanishangaza, hasa ninyi wa makamo,
Watoto mwawatongoza, bila kuwa na kikomo,
Tena mnawapumbaza, kwa kutumia midomo,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

Wengi watu wa heshima, jamii yawaheshimu,
Wana mambo ya kinyama, japo wao wanadamu,
Kila nikiwatazama, wengi hawana nidhamu,
Jione kwenye kioo, uziondoe kasoro.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment