Nazifanya jitihada, japo nipate fursa,
Nifukie hizi shida, na kukomesha mkasa,
Sitojitia kidada, ajira nikiinasa,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Naupiga moyo konde, kutokomeza jazba,
Niishi japo kwa kande, kwani ajira haiba,
Ninalia chondechonde, ukosefu wake mwiba,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Subira yavuta heri, mengi nitavumilia,
Wapo watu mashuhuri, shidani walipitia,
Baba MANDELA jasiri, ni mfano asilia,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Ukiritimba ukwasi, wazua danganyatoto,
Matakwa ya wamilisi, hayajali mchakato,
Ahueni mfilisi, ajira bado fukuto,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Nahisi nimepumbazwa, kama mbuzi wa kafara,
Nazidi kugandamizwa, wao shamrashamra,
Busara zangu zapozwa, zisijezua madhara,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Jirani panikinai, kila siku hekaheka,
Ndugu yangu awa ndui, nifanyacho anicheka,
Mizengwe na kujidai, mtaani asikika,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Mafanikio fahari, kwa wale waliovikwa,
Kuajiriwa johari, kwa walokwisha kuchekwa,
Umaskini jeuri, ndiyo kinga ya kubezwa,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Wengine ni wapagazi, waitafuta riziki,
Wapo na mapaparazi, waganga yao ni dhiki,
Usijivune kwa kazi, siku hazitabiriki,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
Dunia kweli hadaa, walimwengu ni shujaa,
Utajawa na fadhaa, nawe upate wasaa,
Utalopata balaa, maisha kizaazaa,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?
0 comments:
Post a Comment