For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Maisha (Sehemu ya Kwanza)

Dunia naona chungu, siyo sababu majungu,
Sababu ni walimwengu, kuteta yaliyo yangu,
Kisa mie sina changu, mbele yangu ni ukungu,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Ninayo matumaini, siku moja nitapata,
Japo bado ni kizani, na ndoto zenye utata,
Nazidi omba manani, nami tija kuipata,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Mie ni Mtanzania, lazima niwe na nia,
Maisha kupigania, ingawa wanitania,
Kwamba mie ni ngamia, ndivyo walivyonuia,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Ona watoto yatima, wahitaji misaada,
Kila unachokichuma, simalize na vimada,
Tambua hili mapema, wape masikini ada,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Ombaomba mitaani, msaada watamani,
Wenye nacho mkononi, hebu wasaidieni,
Iwe kutoka rohoni, na mola atawapeni,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Wapo walokuwa juu, hivi sasa wako chini,
Watembea kwa miguu, bila kitu mifukoni,
Nguo zao kuukuu, kujificha watamani,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment