For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Jungu Kuu (Sehemu ya pili)


Enyi wana wa mwanangu, nina miaka tisini,
Kufika umri wangu, hakika mnatamani,
Niko kama nungunungu, mwili navyouthamini,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.

Ndugu wajukuu zangu, lazima mjiamini,
Mnavyoishi kizungu, na magonjwa jichungeni,
Msijemeza vichungu, kutumbukia jangani,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.

Mfano ni gonjwa hili, la upungufu wa kinga,
Mkiweza lihimili, mwaka wangu mtatinga,
Na hata mia kamili, haita wapiga chenga,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.

Wajukuu nawasifu, katika hiki kikome,
Shule muwe watiifu, tabia hasi zikome,
Pia muwe wangalifu, na heshima iwe ngome,
Msipende kujisifu, nayo fitina mwichome.

Mwisho ninawakumbusha, nyie taifa la kesho,
Bidii kuionesha, shuleni hisiwe mwisho,
Mifuko kuitunisha, na kuepuka vitisho,
Kumbukeni jungu kuu, hakika lina ukoko.

Mkizingatia haya, mtaishi kama mimi,
Pasipo kuwayawaya, watawaita wasomi,
Nanyi msiwe na haya, kujenga wetu uchumi,
Kumbukeni jungu Kuu, hakika lina ukoko

Leo ninawashukuru, hamjapiga kelele,
Msiwe kama kunguru, enendeni mkalale,
Mkiwa nao udhuru, njooni kama mshale,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment