For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Mama Zetu (Sehemu ya Pili)


Mama machozi futeni, ukombozi umefika,
Msiwe viumbe duni, mwazidi kunyanyasika,
Haki zenu hadi lini? Adha yavuka mipaka !
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Serikali nazo dini, tuacheni ubaguzi,
Yafaa tuwathamini, kwa kuwapa uongozi,
Vyeo tuwapandisheni, popote ngazi kwa ngazi,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Rai nawapa wazazi, nanyi jirekebisheni,
Zigaweni sawa kazi, na pasipo ukinzani,
Chanzo tofauti hizi, huko huko majumbani,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Enyi wanaharakati, wa mambo ya kijinsia,
Iwekeni mikakati, na acheni kusinzia,
Iwe ni yake tamati, unyanyasaji jinsia,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Manani jicho katupa, sote tulione hili,
Mola sikio kakupa, nisikie mara mbili,
Allah ubongo kawapa, tatueni kwa akili,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Kunywa msema maneno, akili mtoa jambo,
Ya jinsia malumbano, sote tuyaweke ng’ambo,
Sheria ni msumeno, ikate huku na huko!
Na wapewe haki sawa, hawa ndio mama zetu

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment