Babu yenu nawaita, njooni kwenye kikome,
Niwape yaliyopita, mtoke kwenye Umeme,
Yasije yakawakuta, miaka yenu ni dume,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Enyi wangu wajukuu, hebu nisikilizeni,
Nami nina mambo makuu, nataka niwambieni,
Kwani bado niko juu, na mwenye matumaini
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Hebu nyote tazameni, huu wangu mkongoja,
Umri wawapiteni, msidhanie porojo,
Nina miaka tisini, waniongoza rojorojo,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Huu weupe kichwani, umeona mambo mengi,
Najua mnatamani, kuishi miaka mingi,
Lakini mtambueni, mbele mnavyo vigingi,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Ninyi wadogo kabisa, tena bado mnasoma,
Hamjakumbwa mikasa, kwenu dunia ni njema,
Machoni kuna vitasa, kila mtu kwenu mwema,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Naanza waelimisha, wajukuu wasichana,
Vishawishi vya maisha, nyie vya wanasa sana,
Malengo vyapukutisha, mtegoni kuwabana,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Ninyi watoto wa kike, masomo zingatieni,
Mabwana wana makeke, mimba wakiwatieni,
Kila siku mkumbuke, mwajingiza matatani,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Mkiwa bado shuleni, wengi mnawavutia,
Kwa mali wawarubuni, tena wakiwasifia,
Jinasue mtegoni, ili msijejutia,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Wengi wa hao mabwana, matapeli wa mapenzi,
Mkisha kubaliana, umejivisha kitanzi,
Mimba mkitunguana, wanakuona mshenzi,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Shuleni mkifukuzwa, kwa wazazi kitimoto,
Mtaani mtatengwa, hata na hao vizito,
Kwa ndugu mtapuuzwa, mtabaki na majuto,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Mimba umri mdogo, kujifungua tatizo,
Yaenda mbio mapigo, kichwani tele mawazo,
Utakufa kama gogo, na kutwachia gumzo,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Pia mwaweza chanika, pindi mnajifungua,
Na yenu ngao kumbuka, subiri mtapokua,
Ungojee lako rika, masomo mkiripua,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Wajukuu wavulana, nanyi pia nawahasa,
Popote mkikutana, muepukeni hanasa,
Mzidi elimishana, kuachana na usasa,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Zingatieni elimu, na mwache udhururaji,
Sikilizeni walimu, wakuze vyenu vipaji,
Wazazi kuwaheshimu, wa mjini na vijiji,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Kumbuka penzi na shule, kimantiki vyapingana,
Mwapaswa kuona mbele, masomo kufundishana,
Nanyi mfike kilele, mafanikio mwanana,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
Vishawishi vya akili, duniani mvikwepe,
Dawa za kulevya mwili, zisiwafanye mapepe,
Na ngono mzikabili, nchi isiwe nyeupe,
Tambueni jungu kuu, hakika lina ukoko.
0 comments:
Post a Comment