For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Nguruwe


Kati ya wanyama wote, nguruwe anichefua,
Nashindwa kumeza mate, kila napomwangalia.

Unajua ni kwanini?, kwa sababu ni mchafu!,
Kwake chochote tumboni, si kwamba namkashifu.

Litazame lake zizi, litakutia kinyaa,
Kulisafisha hawezi, mikono imesinyaa.

Tembo watoa amri, wote wachimbe jalala,
Nguruwe hajihadhari, vichafu ndo anakula.

Choo ameishakanywa, zao kelele hachoshwi,
Na maji anayokunywa, hakika hayachemshwi.

Ukianza kuchunguza, hata kichanja hana,
Ila kinachoshangaza, azidi nenepeana!.

Masika yapofika, zizini kipindupindu,
Kuhara na kutapika, kama kameza ukindu.

Hebu mtazame paka, mwenyewe utasifia,
Kwa miguu afunika, alipojisaidia.

Alala juu ya sofa, pasipo kulichafua,
Ulinzi nampa sifa, panya atufukuzia.

Chakula tunachokula, paka atia kinywani,
Paka ingawa kabwela, usafi yuko makini.

Ewe paka mwelimishe, wako ustaarabu,
Usafi umfundishe, hasingoje matibabu.

Nguruwe ona aibu, mwenyewe umebakia,
Ujinga siwe sababu, balaa kujizulia.

Wito wanyama wenziwe, mnaocheza sambamba,
Kiiga kunya kwa tembo, utapasuka msamba!

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment