Machoni pana kibanzi, nashindwa pata mwafaka,
Naangaza kwa kurunzi, kujaribu kukumbuka,
Mbeleni kuna vitanzi, kichwani nataabika,
Usoni nina simanzi, rohoni nimekereka,
Mwilini ninayo ganzi, jinsi navyosononeka,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Ona janga la Tsunami, kwenye bahari ya hindi,
Mawimbi ya mita kumi, yalopaa kama Bundi,
Yaliathiri uchumi, na yakaua makundi,
Barabara zenye rami, yakatangaza ushindi,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Ajali ya Msagali, Treni zikagongana,
Zote zikawa chakali, mamia zikawabana,
Wengi wakalazwa chali, na ndugu wakatengana,
Sasa tuko nao mbali, japo kufa kufaana,
Tuepusheni ajali, maisha twafupishana,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Ndugu zetu wa Bukoba, meli lienda mlama,
Mawimbi yakawabeba, wengi tukashika tama,
Walofariki si haba, kwenye ziwa walizama,
Wakapoteza mikoba, na mali walizochuma,
Nasi tutoeni toba, tukingojea kiama,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Vita siyo na mantiki, nchi imezivurunda,
Wamepotea malaki, huko Burundi na Rwnda,
Mauaji alaiki, vichwa vingi yaliponda,
Kutwa watu wafariki, kote hofu imetanda,
Ukabila mwahafiki, wahanga warandaranda,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Magofu makuukuu, athari vita za kale,
Wahanga wa vita kuu, wanakovu la milele,
Lipoteza wajukuu, licha ya zao kelele,
Kisa kutaka ukuu, kwa kutumia mishale,
Hasa walokuwa juu, walifanya wasilale,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Vita kuu za Dunia, milioni walikufa,
Wengi waliangamia, katika hayo maafa,
Silaha za nyuklia, zilitumiwa kwa sifa,
Japani wakumbukia, livyotikiswa taifa,
Yiroshima walilia, Nagasaki 'waka-safa',
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Kipindi cha ukoloni, mashujaa walinyongwa,
Walifia vitanzini, wapo pia waloteswa,
Sheria kali barani, hakika zilianzishwa,
Waliwekwa gerezani, muda mwingi walifungwa,
Waliotiwa nguvuni, walikufa kwa kupigwa,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Makamanda FRELIMO, haki mlipigania,
Mapambano na migomo, mwisho vikawakomboa,
Wareno wenye kisomo, walowanyonya raia,
Mkawaziba midoma, ulaya wakarejea,
Mateso yana kikomo, na sasa mko huria
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Ushindi wenu ni tunu, hamtosahaulika,
Ufanisi nazo mbinu, vyote tutavikumbuka,
Wapiganaji wa ZANU, popote mwaheshimika,
Majemedari wa KANU, barani mnasifika,
Propaganda za TANU, kamwe hazitobanduka,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
MANDELA nae NUJOMA, Kusini hawakuchoka,
Makaburu walogoma, mwishoe wakang’atuka,
Mabeberu wenye njama, wakaacha madaraka,
Nae hayati NKURUMA, uhuru aliusaka,
Kidete akasimama, kunganisha Afrika,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Wazawa wa MAUMAU, mlipinga Ukoloni,
Ulozidisha dharau, unyama uso kifani,
MKWAWA kapiga mbiu, kwondosha wajerumani,
Tabia za kinyang’au, kutokomezwa nchini,
Mabadiliko ndo kiu, mliyapata vitani,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Wahanga wa MAJIMAJI, milele ni kama taa,
Wastaili mataji, jinsi walivyoshujaa,
Vijana wapiganaji, vitani walishupaa,
Wazawa wana-vijiji, pamoja wakakataa,
Unyama na mauaji, jinsi yalivyozagaa,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Mauaji ya SOWETO, wengi yalipukutisha,
Weusi kwao msoto, makaburu wawendesha,
Upondaji wa kokoto, weusi uliwatisha,
Wa mlengo wa kushoto, vurugu wakaanzisha,
Kila siku mkong’oto, maisha wayakatisha,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Juhudi mwazifahamu, ndugu zetu Nigeria,
Damu zenu zitadumu, Angola na Tunisia,
Manani awarehemu, wenzetu Algeria,
Heko mlomwaga damu, uhuru kujipatia,
Usawa wa binadamu, Afrika kutetea,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Mioyo yenu shupavu, haina wake mfano,
Mili ya ukakamavu, ulitii mapigano,
Mkapigana kwa nguvu, bila kujali maneno,
Mkayapisha mafuvu, kukabili mapambano,
Wageni kushika shavu, na kusaga yao meno,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
Majonzi yana utata, poleni yalowafika,
Ya ugonjwa au vita, waso-hatia kifyeka,
Mitima inafukuta, wapendwa wakitutoka,
Ubongo utatokota, upweke ukiuteka,
Vumbini tajikokota, kichwani kisononeka,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.
0 comments:
Post a Comment