Leo jioni tulivu, mekaa chini ya mti,
Pepo zavuma kwa nguvu, kibaridi kikokati,
Majani yote makavu, Banda langu la Makuti,
Macho bado maangavu, nikipanga mikakati.
Nawaza nakuwazua, lini nitakuwa juu?
Wajuu wanizuzua, ingawa sina makuu,
Na panga na kupangua, hali hii yanikifu,
Fukara najitambua, japo moyo mkunjufu.
Mbali namwona jirani, aja kwa kuyumbayumba,
Yuko hoi taabani, miguu imemvimba,
Anapofika nyumbani, kafungua kimkoba,
Hakika ni maskini, hana alichokibeba.
Kumbuka huyu mwenzangu, anao wake wawili,
Japo maisha machungu, ataka kuleta mwali,
Tena kutoka marangu, bila kuwa na mahali,
Ajapo nyumbani kwangu, gongo anuka kwa mbali.
Watoto walalamika, hawana kitu tumboni,
Mwenye nyumba amefika, Kodi yake haioni,
Mifuko imetatuka, kujificha atamani,
Machoni yabubujika, namrumia jirani.
Bado niko kivulini, wapita wapita-njia,
Wote tabaka la chini, wakitoka kuhemea,
Wengine wana huzuni, kuna jambo wajutia
Wenye chupa mkononi, ndo walionivutia.
Wazee hawa wawili, pombe zimewapembua,
Wametembea umbali, bila ya kujitambua,
Wote walevi chakali, njiani wajikakamua,
Vinywani moshi mkali, Bangi zimewabangua.
Kelele mji mzima, shida kutozikumbuka,
Ki-vipato wako nyuma, maisha wachakarika,
Wote ukiwatazama, mwili mzima viraka,
Watoto hawatosoma, pombe ada yatumika.
Wana-mitara nyumbani, japo yamewachachia,
Ni wao utamaduni, vilabuni kwa-mkia,
Matusi tele vinywani, unapowaangalia,
Nyusoni hawana soni, kutwa pombe wanukia.
Wamejijengea jadi, mithili ya vipepeo,
Jioni wanaporudi, wake wapigwa vibao,
Wasidhani wafaidi, nao wana haki zao,
Kuacha hawana budi, na kukua kiupeo.
Gafla ninagutuka, kibandani kunavuja!
Juzi tu nimehezeka, siku mbili tu kioja!
Makuti yanapenyeka, ninalowa bila haja,
Kweli ninasafarika, njiani najikongoja.
Nabakia kuwazia, hali yao ndiyo yangu,
Maisha yetu sawia, nakula pia vichungu,
Sina cha kuwatambia, umaskini ni pingu,
Ni wapi nitaanzia, nami nipo kwenye wingu?!
0 comments:
Post a Comment