Tembelea vijijini, ushirikina ni hofu,
Wananchi tambueni, imani hii potofu,
Mauwaji yaacheni, vikongwe wawapungufu,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Wameibuka magangwe, wazee waangamiza,
Wanaoua vikongwe, ni uchawi watangaza,
Chanzo cha hii mizengwe, macho mekundu wabeza,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Wahuni wana magenge, ya madawa ya kulevya,
Vijana msijidunge, na mwepuke kuyachovya,
Msivagae mkenge, jihadhari kimya kimya,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo
Tuwabane wauzaji, na watumiaji wote,
Wengi wako kwenye miji, wawajibishwe popote,
Na wale wadhururaji, wasiyamezee mate,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Dini zatusikitisha, migongano sasa tele,
Katika yetu maisha, mola tumuweke mbele,
Upendo kuudumisha, tuache kuyumba milele,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Imani yetu nchini, kuabudu tuko huru,
Migogoro ya kidini, inaweza kutudhuru,
Kutupokonya amani, kama kuku kwa kunguru,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
0 comments:
Post a Comment