Pombe hadi saa sita, uchumi humo kizani,
Wa gongo mwawakamata, hawapandi kizimbani?
Tupige ulevi vita, chanzo cha umaskini,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Waume kwa wanawake, muda mwingi vilabuni,
Kazi wazipiga teke, mchana pombe vichwani,
Watembea kwa makeke, watoto wako njaani,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Tathimini wako moyo, epuka hulka hasi,
Ulafi nao uchoyo, hizi tabia za fisi,
Tabia uliyonayo, ipukutishe kwa kasi,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Wapo pia wanafiki, nduguze ubinafsi,
Akili zao fataki, wapendelea maasi,
Hawa nao tuwamaki, mwenendo wao ni hasi,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Wengi kwenye jumuiya, waendekeza dhuruma,
Mwenendo huu mbaya, wakumba hata yatima,
Wahusika mwone haya, hii sifa ya kinyama,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Na ninyi wenye dharau, pia wapenda ugomvi,
Tabia zetu limau, zichanganywapo na chumvi,
Ziacheni angalau, kabla ya zenu mvi,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Huduma kwao wajane, hakika tuzingatie,
Pamoja tushikamane, majonzi tuwafutie,
Waajiri tuwabane, mafao wawapatie,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
Yangu dira mkubali, kwani tumo safarini,
Kumbuka twendako mbali, hasa ninyi wa angani,
Na hizi rai kauli, ziwekeni akilini,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.
0 comments:
Post a Comment