For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Dira (Sehemu ya Tatu)

Tuwe macho duniani, na kung’aa kwa mwili,
Kuna walozua fani, iitwayo utapeli,
Mabazazi wa nchini, ndiyo miradi kamili!,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.

Ona madereva wetu, gari la Umma ni lao,
Kutwa mara tatu tatu, ndilo lao azimio,
Kwa nini wanathubutu, na yupi ni kimbilio?
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.

Chunguza mali ya Umma, nasi ututaarifu,
Waipitisha kwa nyuma, mwaita wabadhirifu,
Sheria itawazima, kwani pia waharifu,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.

Kila mtu augua, kwanini mnashangaa?
Wagonjwa mwawabagua, eti mwaona kinyaa,
Yawabidi kutambua, si utu kunyanyapaa,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.

Zichunguze zetu kaya, utafumba macho yako,
Mwisho utaona haya, kwa hayo maangaiko,
Wanyanyasika vibaya, kisa virusi ni mwiko,
Hii ndiyo dira yetu, kubali wake mwongozo.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment