Nami nalodukuduku, nalo ukera mtima,
Ingawa sijajishuku, chombo chaenda mlama,
Maneno kama chiriku, siyo chanzo cha neema,
Uchezaji wa mapiku, waipunguza rehema
Walimwengu tuwe macho, kuepusha dukuduku.
Kamtindo kamezuka, wenye kura kukirimu,
Wale tuliopevuka, huu siyo ukarimu,
Ona pirikapirika, wote wataka kudumu,
Kwa wanaokurupuka, machoni watiwe ndimu,
Takrima ni adui, sawa na kidudu mtu.
Dhana yake yapotoshwa, na wale wanaopwaya,
Wengi wetu tumechoshwa, kwa hizo fikra boya,
Wanafaa kunyooshwa, waache kuwayawaya,
Takrima nayo rushwa, kama umeme na nyaya,
Takrima ni adui, sawa na kidudu mtu!
Kila atowaye kitu, kuna jambo atafuta,
Vichwani ajaza kutu, tudhani ametameta,
Kumbe ana ukurutu, anang’aa kwa mafuta,
Sirika hii ni butu, tunapaswa kuifuta,
Takrima ni adui, sawa na kidudu mtu.
Kuna kitu wahitaji, kwa kujifanya ni wema,
Njuruku pia vinywanyi, wagawa bila kuhema,
Wapitapo kwenye miji, jembe na chumvi mwachuma,
Watubana kienyeji, pasipo tambua njama,
Takrima ni adui, sawa na kidudu mtu.
0 comments:
Post a Comment