For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Maisha bila Ajira (Sehemu ya Nne)

        Ratiba yangu kwa siku, yasawiti wazi dhiki,
Mara kule mara huku, ndipo nipate riziki,
Mchakato naushuku, kasoro hazitibiki,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Jamaa anilaghai, niendelee kuishi,
Dawa ya mlalahoi, kutumia ushawishi,
Ufukara ni adui, japo mwatia nakishi,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Asubuhi naamka, kichwa chawaza ajira,
Nishie nae kumbuka, ni kaka yake na mama,
Mwenye ukwasi hakika, na kazi ya kumripa,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Kazini anapokwenda, pamoja na mke wake,
Majukumu naachiwa, jamani niwambieje,
Mpate sadiki haya, yanayonipa kiwewe,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Mosi, ninapoamka, magari ninasafisha,
Watoto huwaandaa, shuleni waweze kwenda,
Jinsi walivyodekezwa, mwenzenu nimeshachoka,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Pili, sokoni huenda, mahitaji kununua,
Huko ninaowakuta, wote ni akina mama,
Hakika hunishangaa, sokoni ninapoenda,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Nguo zao nazifua, nakupiga pasi pia,
Ifikapo saa saba, shuleni nahitajika,
Watoto kuwachukua, nyumbani kuwafikisha,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Maji yakisha-katika, nahitajika kusomba,
Mengi yameshanikuta, siwezi yote eleza,
Namlilia yehova, shidani kuniepusha,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Hata kidato cha sita, elimu niliyonayo,
Tena gredi ya kwanza, yafaa kuajiriwa,
Popote pale kwa muda, kabla ya chuo kwenda,
Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Singependa fadhaika, na kupatwa matatizo,
Ubongo kutiwa doa, nikiwa kijana bado,
Niepushe uloguswa, leo kwangu kesho kwako!
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

Wito nautoa kwenu, mliofanikiwa sasa,
Msinyanyase wenzenu, kwani maisha mlima,
Tuchezeni kama timu, pasipo kubaguana,
  Maisha bila ajira, nifanyeje walimwengu?

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment