For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Maisha (Sehemu ya Pili)

Safari bado ni ndefu, sijione mtukufu,
Tabia za ushaufu, wenzio zinawakifu,
Ufahari sifa mfu, usipende kujisifu,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Waona tope wenzio, kisa kumiliki gari,
Maisha kikaangio, punguza yako jeuri,
Ulapo vipapatio, sitafune kwa kiburi,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Simcheke mlemavu, hujui mtondogoo,
Jifunze unyenyekevu, sijifanye komandoo,
Ukwasi wakupa nguvu, kudhani wenzio choo,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Kuna watu tegemeo, wana roho ya kwanini!,
Kwani tajiri wa leo, kesho ndiye masikini,
Tuishi kama kondoo, tukafaidi peponi,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Kuna watu wana njaa, wachache wala wasaza,
Wapita kwenye mitaa, waloshiba wakubeza,
Wengi wakata tama, kutwa nzima wanawaza,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

Zangu rai nimetoa, mwanadamu jitambue,
Zako kasoro ondoa, wenye shida uwafae,
Umaskini ni doa, jamii ijikomboe,
Maisha ndivyo yalivyo, kupanda pia kushuka.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment