For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Kizunguzungu


Nami leo nalo swali, naomba mnipe jibu,
Nataka kupata mwali, tabia yake dhahabu,
Najaribu kusahili, lakini sina jawabu,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Katika jamii yetu, wapo wengi wasichana,
Tabia zao za chatu, hawapendi kutafuna,
Wengi wao watukutu, wana wengi mabwana,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Nataka Binti mweusi, nashangaa simpati!,
Japo waishi na sisi, wajifanya tofauti,
Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Wapo wenye mikorogo, utadhani waasia,
Wajipanga mlolongo, saluni kujipodoa,
Wengi wao ni waongo, wahitaji wenye nia,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Mavazi yanichukiza, nusu uchi wanavaa,
Miili wanaiuza, utadhani ni vichaa,
Mi bado najiuliza, wanatafuna milaa,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Nikioa kijijini, ‘aweza-chenji’ mjini,
Na akawa limbukeni, wakunitia shidani,
Wenye mali kutamani, penzi kuwa kitanzini,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Na hao wa geti-kali, naogopa kudekewa,
Pia kuzibwa kauli, na shidani kukimbiwa,
Kwani palipo ukweli, uongo utenguliwa,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Msomi ningetafuta, lakini ni wasumbufu,
Watembeapo hunata, na wapenda kujisifu,
Mali mtakapopata, hujiona wakamilifu,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Meangaza duniani, bado sijapata wangu!
Japo mwili watamani, roho yaweka kiwingu,
Hakika nimeamini, mapenzi kizunguzungu!
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Kumbuka mie fukara, wengi wanataka fedha, 
Nami na pesa uchwara, kuishi nao ni adha,
Penzi lisije nikera, ninaomba mawaidha,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Tambua mie mgumu, sipendi wakunitenda,
Nisijepatwa wazimu, na kuapa kutopenda,
Nikaja kukosa hamu, mapenzi kutoyapanda
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Mapenzi yanitatiza, kaka yenu sijiwezi,
Warembo wanikonyeza, ninahisi wapuuzi,
Fikra zanikataza, je niachie wazazi?
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Nimebaki njia panda, sioni wakumpenda,
Kila ninaemuwinda, moyo wangu wamponda,
Miaka mbio yaenda, nani moyo taushinda?
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

Kirika nashawishika, kujitia mawindoni,
Kabla sijapotoka, zenu nasaha toeni,
Kalamu naitundika, yetu mawazo nipeni,
Mie nimpende nani, na kwanini nimpende?

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment