For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Karibuni Tanzania

Mito mithili ya nyoka, bondeni yatiririka,
Yakunja na kukunjuka, sauti tamu yasikika,
Nyikani yabubujika, rangi nzuri yachipuka,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Tazama yake mandhari, hakika utavutiwa,
Pepo nzuri za bahari, maji matamu ya ziwa,
Nyuso zenye utayari, nchini utapokewa,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Wanyama tele mbugani, Duniani wasifika,
Twiga warefu nchini, kama nembo watumika,
Sokwe-mtu nao nyani, wanyama wenye pilika,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Visiwani panukia, marashi ya karafuu,
Hujambo! Wakwamkia, wote ni wachangamfu,
Vivutio asilia, vyapendeza maradufu,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Wadudu pia mimea, nchi yeu waipamba,
Kijani iloenea, yapendezesha mashamba,
Ndege walonenepea, amani yetu waimba,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Makabila yapo mengi, na hakuna ubaguzi,
Hatujigawi kwa rangi, twachukia uchochezi,
Ucheshi ndio msingi, hatupendi uchokozi,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Kiswahili lugha tamu, ndiyo lugha ya taifa,
Kiungo cha ukarimu, pasipo kuleta ufa,
Chasukuma gurudumu, na kujenga utaifa,
Karibuni Tanznaia, nchi inayopendeza.

Mwenge wetu wa uhuru, chemichemi ya amani,
Nchini watoa nuru, hata kwa ninyi wageni,
Amani kutokufuru, kwetu ni utamaduni,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Mlima Kilimanjaro, paa letu Africa,
Unakinga migogoro, Tanzania kuibuka,
Zikitokea kasoro, barafu yazifunika,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Kwa usawa twatukuka, haki kuipigania,
Kusini mwa Afrika, uhuru tulitetea,
Wadhalimu kuwafyeka, barani kutokomea,
Karibuni Tanzania, nchi inayopendeza.

Utamaduni asili, Tanzania twautii,
Mila zetu mbalimbali, zavutia watalii,
Najua mnakubali, kabila la WAMASAI,
Karibuni Tanzania, Kisiwa chenye amani.

Maporomoko ya maji, ardhini yarindima,
Karibu wawekezaji, kwenye nchi nayovuma,
Penye miji na vijiji, na watu wenye karama,
Karibuni Tanzania, Mfurahie amani.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

Amani Tanzania

Leo tunayofuraha, kuitwa watanzania,
Kwa amani twatukuka, hata nje ya mipaka,
Mazingira yasifika, wageni yawavutia,
Nchi ya kiafrika, ya watu wenye hamasa,
Tusichezee amani, kwenye shimo la choo.

Ona Rwanda na Burundi, amani waitamani,
Hawataki ukimbizi, wapenda pia amani,
Tuepuke uchochezi, wa kuleta tafurani,
Takayoleta Tsunami, kututenga na amani,
Tusichezee amani, kwenye shimo la choo.

Tushukuru waasisi, wa hii yetu amani,
Kambarage tumuenzi, pia Mzee Amani,
Mola hatotubariki, kama hatuwakumbuki,
Walitoa jasho jingi, amani kuiasisi,
Tusichezee amani, kwenye shimo la choo

Elewa neno ‘amani’, kinyume chake ni ‘vita’,
Gharama yake ni kali, ukitaka irudisha,
Kama huwezi amini, nenda Kongo kuuliza,
Hebu fikeni Sudani, na angaza Liberia,
Tusichezee amani, kwenye shimo la choo.

Vita kama tindikali, katika nyingi jamii,
Taparaganya uchumi, kwongeza umasikini,
Kila siku mafichoni, bila ya kwenda kazini,
Mzalendo tafakari, kabla ya tafrani,
Tusichezee amani, kwenye shimo la choo.

Mito tiririke maji, sipendi kuona damu,
Waafrika jamani, kunani huko Ikulu?
Vita chanzo chake nini, madaraka ndiyo chachu?
Twiga semeni amani, nisingependa vulugu,
Tusichezee amani, kwenye shimo la choo.

Uchaguzi utafika, yetu demokrasia,
Siyo bola kuchagua, chagua aliye bora,
Wengi twamuomba mola, atupe aliye bora,
Amani kuidumisha, ije kuwa yake dira,
Tusichezee amani, wenzetu wanaisaka.

Tuondoe tofauti, ziletazo utengano,
Tubaini wanafiki, wenye uchu na mizozo,
Vichwani wajaza chuki, ubabe na malumbano,
Hakika ni mamluki, waletao migongano,
Tusichezee amani, wenzetu wanaisaka.

Ni vyema nchi wahame, wasotutakia mema,
Wasifanye tukosane, amani kutuponyoka,
Vibaraka waondoke, nia yao siyo njema,
Wenye chuki wapatane, kutuepushia vita,
Tusichezee amani, wenzetu wanaisaka.

Nchi yangu Tanzania, duniani wasifika,
Neema nakuombea, Amani kuimarika,
Wenye hila kupotea, bila damu kumwagika,
Migogoro kufagia, utuliu kuchipuka,
Tusichezee amani, wenzetu wanaisaka.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

Buriani: Machozi

Machoni pana kibanzi, nashindwa pata mwafaka,
Naangaza kwa kurunzi, kujaribu kukumbuka,
Mbeleni kuna vitanzi, kichwani nataabika,
Usoni nina simanzi, rohoni nimekereka,
Mwilini ninayo ganzi, jinsi navyosononeka,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Ona janga la Tsunami, kwenye bahari ya hindi,
Mawimbi ya mita kumi, yalopaa kama Bundi,
Yaliathiri uchumi, na yakaua makundi,
Barabara zenye rami, yakatangaza ushindi,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Ajali ya Msagali, Treni zikagongana,
Zote zikawa chakali, mamia zikawabana,
Wengi wakalazwa chali, na ndugu wakatengana,
Sasa tuko nao mbali, japo kufa kufaana,
Tuepusheni ajali, maisha twafupishana,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Ndugu zetu wa Bukoba, meli lienda mlama,
Mawimbi yakawabeba, wengi tukashika tama,
Walofariki si haba, kwenye ziwa walizama,
Wakapoteza mikoba, na mali walizochuma,
Nasi tutoeni toba, tukingojea kiama,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Vita siyo na mantiki, nchi imezivurunda,
Wamepotea malaki, huko Burundi na Rwnda,
Mauaji alaiki, vichwa vingi yaliponda,
Kutwa watu wafariki, kote hofu imetanda,
Ukabila mwahafiki, wahanga warandaranda,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Magofu makuukuu, athari vita za kale,
Wahanga wa vita kuu, wanakovu la milele,
Lipoteza wajukuu, licha ya zao kelele,
Kisa kutaka ukuu, kwa kutumia mishale,
Hasa walokuwa juu, walifanya wasilale,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Vita kuu za Dunia, milioni walikufa,
Wengi waliangamia, katika hayo maafa,
Silaha za nyuklia, zilitumiwa kwa sifa,
Japani wakumbukia, livyotikiswa taifa,
Yiroshima walilia, Nagasaki 'waka-safa',
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.


Kipindi cha ukoloni, mashujaa walinyongwa,
Walifia vitanzini, wapo pia waloteswa,
Sheria kali barani, hakika zilianzishwa,
Waliwekwa gerezani, muda mwingi walifungwa,
Waliotiwa nguvuni, walikufa kwa kupigwa,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Makamanda FRELIMO, haki mlipigania,
Mapambano na migomo, mwisho vikawakomboa,
Wareno wenye kisomo, walowanyonya raia,
Mkawaziba midoma, ulaya wakarejea,
Mateso yana kikomo, na sasa mko huria
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Ushindi wenu ni tunu, hamtosahaulika,
Ufanisi nazo mbinu, vyote tutavikumbuka,
Wapiganaji wa ZANU, popote mwaheshimika,
Majemedari wa KANU, barani mnasifika,
Propaganda za TANU, kamwe hazitobanduka,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

MANDELA nae NUJOMA, Kusini hawakuchoka,
Makaburu walogoma, mwishoe wakang’atuka,
Mabeberu wenye njama, wakaacha madaraka,
Nae hayati NKURUMA, uhuru aliusaka,
Kidete akasimama, kunganisha Afrika,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Wazawa wa MAUMAU, mlipinga Ukoloni,
Ulozidisha dharau, unyama uso kifani,
MKWAWA kapiga mbiu, kwondosha wajerumani,
Tabia za kinyang’au, kutokomezwa nchini,
Mabadiliko ndo kiu, mliyapata vitani,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Wahanga wa MAJIMAJI, milele ni kama taa,
Wastaili mataji, jinsi walivyoshujaa,
Vijana wapiganaji, vitani walishupaa,
Wazawa wana-vijiji, pamoja wakakataa,
Unyama na mauaji, jinsi yalivyozagaa,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Mauaji ya SOWETO, wengi yalipukutisha,
Weusi kwao msoto, makaburu wawendesha,
Upondaji wa kokoto, weusi uliwatisha,
Wa mlengo wa kushoto, vurugu wakaanzisha,
Kila siku mkong’oto, maisha wayakatisha,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.


Juhudi mwazifahamu, ndugu zetu Nigeria,
Damu zenu zitadumu, Angola na Tunisia,
Manani awarehemu, wenzetu Algeria,
Heko mlomwaga damu, uhuru kujipatia,
Usawa wa binadamu, Afrika kutetea,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Mioyo yenu shupavu, haina wake mfano,
Mili ya ukakamavu, ulitii mapigano,
Mkapigana kwa nguvu, bila kujali maneno,
Mkayapisha mafuvu, kukabili mapambano,
Wageni kushika shavu, na kusaga yao meno,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

Majonzi yana utata, poleni yalowafika,
Ya ugonjwa au vita, waso-hatia kifyeka,
Mitima inafukuta, wapendwa wakitutoka,
Ubongo utatokota, upweke ukiuteka,
Vumbini tajikokota, kichwani kisononeka,
Buriani mlokufa, mwenyezi awarehemu.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

Wapita Njia

Leo jioni tulivu, mekaa chini ya mti,
Pepo zavuma kwa nguvu, kibaridi kikokati,
Majani yote makavu, Banda langu la Makuti,
Macho bado maangavu, nikipanga mikakati.

Nawaza nakuwazua, lini nitakuwa juu?
Wajuu wanizuzua, ingawa sina makuu,
Na panga na kupangua, hali hii yanikifu,
Fukara najitambua, japo moyo mkunjufu.

Mbali namwona jirani, aja kwa kuyumbayumba,
Yuko hoi taabani, miguu imemvimba,
Anapofika nyumbani, kafungua kimkoba,
Hakika ni maskini, hana alichokibeba.

Kumbuka huyu mwenzangu, anao wake wawili,
Japo maisha machungu, ataka kuleta mwali,
Tena kutoka marangu, bila kuwa na mahali,
Ajapo nyumbani kwangu, gongo anuka kwa mbali.
Watoto walalamika, hawana kitu tumboni,
Mwenye nyumba amefika, Kodi yake haioni,
Mifuko imetatuka, kujificha atamani,
Machoni yabubujika, namrumia jirani.

Bado niko kivulini, wapita wapita-njia,
Wote tabaka la chini, wakitoka kuhemea,
Wengine wana huzuni, kuna jambo wajutia
Wenye chupa mkononi, ndo walionivutia.

Wazee hawa wawili, pombe zimewapembua,
Wametembea umbali, bila ya kujitambua,
Wote walevi chakali, njiani wajikakamua,
Vinywani moshi mkali, Bangi zimewabangua.

Kelele mji mzima, shida kutozikumbuka,
Ki-vipato wako nyuma, maisha wachakarika,
Wote ukiwatazama, mwili mzima viraka,
Watoto hawatosoma, pombe ada yatumika.

Wana-mitara nyumbani, japo yamewachachia,
Ni wao utamaduni, vilabuni kwa-mkia,
Matusi tele vinywani, unapowaangalia,
Nyusoni hawana soni, kutwa pombe wanukia.

Wamejijengea jadi, mithili ya vipepeo,
Jioni wanaporudi, wake wapigwa vibao,
Wasidhani wafaidi, nao wana haki zao,
Kuacha hawana budi, na kukua kiupeo.

Gafla ninagutuka, kibandani kunavuja!
Juzi tu nimehezeka, siku mbili tu kioja!
Makuti yanapenyeka, ninalowa bila haja,
Kweli ninasafarika, njiani najikongoja.

Nabakia kuwazia, hali yao ndiyo yangu,
Maisha yetu sawia, nakula pia vichungu,
Sina cha kuwatambia, umaskini ni pingu,
Ni wapi nitaanzia, nami nipo kwenye wingu?!

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS