For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Tausi


Nimezunguka mwituni, pasipo kutarajia,
Na sikuwa mawindoni, basi ndege kanijia,
Jinale tausi-jani, mwenyewe kanitajia,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Nikachunguza umbole, likanitia wazimu,
Sikuwahi penda kale, huyu ndege muhimu,
Nimeandaa mishale, kumtupia kwa zamu,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Ewe tausi mrembo, kweli umependelewa,
Nionapo lako umbo, hakika umejaliwa,
Kichwani bado ni fumbo, ni wapi umezaliwa?
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Tausi ndege mzuri, mrembo wa kuvutia,
Wang’aa kama Hariri, mwanga waniangazia,
Mwangaza wa kibatari, tena usiofifia,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Shingo mithili ya twiga, yavuta kama sumaku,
Mboni zako za kichaga, ni sawa na za chiriku
Mwendo wako wa kinyonga, wazidisha dukuduku,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!
Katika kundi la ndege, wewe ndiye malkia,
Hata kanga wakuige, robo hawatofikia,
Mikorogo wakoroge, rangi yako asilia,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Sauti yako nyororo, kama nyuzi za gitaa,
Mie napata kihoro, sawa na giza kwa taa,
Tujifunge minyororo, tupite kila mtaa,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Mzuri mwenye adabu, vijana wakutafuta,
Japo huvai dhahabu, kizani wameremeta,
Mvuto wako dhawabu, upweke utanifuta,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Mlimbwende wa dunia, mabawa ya almasi,
Macho nikikwangazia, wewe ni lulu tausi,
Hakika nimepania, hebu toa wasiwasi,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Mawazo ni kimbiliyo, yadhihirisha bidii,
Tabia uliyonayo, yanivuta kwa utii,
Kwako nitasema ndiyo, uwamuzi sijutii,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Nisemacho ni sahihi, na wala siko peponi,
Moyo wangu wafurahi, kwa yako rangi mwilini,
Nikwonapo asubuhi, najihisi burudani,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Jinsi unavyorembua, wanifanya niwe hoi,
Tausi wanisumbua, japo siri sitoboi,
Yakubidi kutambua, ngozi yako kama toi,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Kichwa chazidi niuma, mwenzio sina ruzuku,
Upitapo nainama, mwenzako mie kasuku,
Kisha najishika tama, usinitoe mkuku,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Mtima wafadhaika, kwangu ua waridi,
Ninashindwa kutamka, japo sipendi kuwadi,
Midomo yatetemeka, sipati hoja jadidi,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Tuwe sote mawinguni, unaporuka hewani,
Tuitunze bustani, ua lichipue chini,
Kisha nione usoni, penzi latoka moyoni,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Kila tunapokutana, macho tunakaziana,
Kihisia twapendana, kunena twaogopana,
Mikono tukishikana, twaduwaa kuachana,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Sitaki nimtizame, anifanye nikumbuke,
Naye hataki nihame, roho isifadhaike,
Penzi ni kama umeme, ushikapo nyaya zake,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Anipigia kinanda, kihisia niko kati,
Mawazo yarandaranda, napo panga mikakati,
Sasa niko njia panda, japo napenda kwa dhati,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Nampenda maradufu, nataka awe wa kwangu,
Penzi ni kama upofu, mbele naona ukungu,
Rohoni ninayo hofu, nahisi kizunguzungu,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Napokuona usoni, kuna jambo walificha,
Nipe yaliyo rohoni, pendo lisije kuchacha,
Nong’oneze sikioni, nikufanye wangu kocha,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Mtima umeushinda, haunalo pingamizi,
Tazama nilivyokonda, mithili ya sisimizi,
Sababu ninakupenda, na sipendi kuwa wazi,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Tuweke wazi hisia, milele tuwe pamoja,
Mashoga kuwasusia, pendo lisije kuchuja,
Kuzingatia wosia, iwe ngao ya vihoja
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Unipende tupendane, tusendelee fichana,
Nasi tukubaliane, pasipo haya kuona,
Popote tushikamane, kama mapacha vijana,
Kuwa nawe natamani, ingawa mie mgumu!

Naomba nitamkie, uniondoe shidani,
Watu wote watambue, tumeungana rohoni,
Hisia tuzifichue, tutaficha mpaka lini?
Najua tunapendana, tuweke hisia wazi!

Mara ndoto yanijia, pamoja tuko peponi,
Pete wanizawadia, na kunibusu shavuni,
Nami nakukumbatia, na kuvisha kidoleni,
Tuifanye ndoto kweli, popote tuambatane.

Twaogelea bwawani, jua latoa miali,
Furaha tele rohoni, naona kitendawili,
Katika mabilioni, tumesimama wawili!
Oooh tausi mzuri, wewe ni Ua waridi.

Tazama bustanini, Ua pendo lachanua,
Kulichuma natamani, macho waniangazia,
Mwenzio sioni soni, moyo umekuchagua,
Mawazoni ndiwe nyota, tokea alfajiri.

Hebu nione machoni, kuna upendo wa dhati,
Nitazamapo pichani, kifikra huwa kati,
Ni wewe tu duniani, meniteka kwa manati,
Niruhusu nikupende, ndoani tuwe mfano.

Tausi macho yafunge, kurasa mpya fungua,
Dengua kwa vitatange, penzi kutolitengua,
Warembulie vingunge, hila zao kupangua,
Liruhusu pendo langu, doani tuwe mfano.

Tausi kakamilika, mvuto wa kimahaba,
Akipita nagutuka, kaniganda kama ruba,
Nikimwona nazimika, analo jicho la huba,
Ingawa mie mgumu, hisia umeziteka!

We kidani cha nafsi, wengine sina nafasi,
Ingawa wananighasi, Waarabu kwa watusi,
Hawanipi wasiwasi, nimekupenda tausi,
tokea alfajiri, Mawazoni ndiwe nyota.

Zivae zako chachandu, ujivike na ushungi,
Shanga zako za kihindu, zanikuna mara nyingi,
Mboni zako za utundu, kama binti wa kirangi,
Liruhusu pendo langu, ndoani tuwe mfano.

Unikunapo kidevu, nahisi nina bahati,
We sehemu ya ubavu, sina tena kizingiti,
Tuwe sote nchi kavu, tupae kwa parachuti,
Ingawa mie mgumu, hisia umeziteka!

Tausi waniumiza, mwili wautetemesha,
Kutwa nzima kukuwaza, mtima wautonesha,
Macho unavyolegeza, Urembo wauboresha,
Ingawa mie mgumu, hisia umeziteka!

Nasi tuwe wawazi, tangazo kwenye mimbali,
Upendo wa wiziwizi, waipunguza morali,
Tufahamishe wazazi, ili watupe kibali,
Tuwe mithili ya njiwa, anga wawiliwawili.

Kanisani tufichue, huku twavuta subira,
Hata rafiki wajue, rohoni ndiwe kinara,
Ndugu nao watambue, pete itoe ishara,
Tuwe mithili ya njiwa, anga wawiliwawili.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment