For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Siku ya Wapendanao Mpwapwa


MPWAPWA sehemu nzuri, yenye upepo mwanana,
Ukichunguza mandhari, milima inapishana,
Kipindi cha hadhuhuri, mvuto waonekana,
Penye wengi pana mambo.

Tukiwa Mpwapwa shule, vijana tulikutana, 
Na WAGUMU tupo pale, kisera tunapatana,
WALAINI vile vile, wa kike kwa wavulana,
Penye wengi pana mambo.

Ngoja niwapeni kisa, cha WALAINI watatu,
Vijana wana Usasa, wakipigana viatu,
Pasipo kutoa posa, shule mihula mitatu,
Penye wengi pana mambo.

Ni wavulana wawili, kwa msichana mmoja,
Japo watokea mbali, twasoma nao pamoja,
Kwa binti wako chakali, wote kidato kimoja,
Penye wengi pana mambo.

Wa kike jinale Gati, Mzuri wa Wastani,
Mboji na mwenzie Joti, binti wakamtamani,
Wakayapiga magoti, awaumiza rohoni,
Penye wengi pana mambo.

Joti kwao kwenye jiji, ufukara wamkwaza,
Mwenzake kijana mboji, kifedha alijiweza,
Hakusita ‘kuzifoji’, mrembo kumlegeza,
Penye wengi pana mambo.

Wote wakamtongoza, Gati hakuwakataa,
Nasi tulipochunguza, binti kawapa ridhaa,
Mmoja katueleza, mototo anatamaa,
Penye wengi pana mambo.

Penzi lao likadumu, wakiwa naye sambamba,
Watesa nae kwa zamu, japo kawafunga kamba,
Hawakuwa kwenye damu, ingawa hawakuyumba,
Penye wengi pana mambo

Tukafanya utafiti, binti ana lake jambo,
Eti alipenda Joti, sababu ya lake umbo,
Mboji kupendewa noti, na dada huyo mrembo,
Penye wengi pana mambo.

Wawili awachanganya, pasipo wao kujua,
WAGUMU tukawakanya, japo walitutimua,
Kimwana awadanganya, bila ya kujigundua,
Penye wengi pana mambo.

Gati ndumila kuwili, penzini kawanasa,
Waume wote wawili, pasipo kujitikisa,
Kikawa kitendawili, nani talamba galasa?
Penye wengi pana mambo.

Mwezi wa pili ukaja, tarehe kumi na nne,
Ni yupi wawe pamoja, siku ya jumanne,
Gati hana ujanja, kipindi cha saa nane,
Penye wengi pana mambo.
   
Siku ya siku mefika, naona nyekundu nguo,
Vijana wamepambika, kwa mavazi ya kileo,
WAGUMU twataabika, SIKU YA WAPENDANAO,
Penye wengi pana mambo

Sote twaweka mkazo, kwake Gati na vijana,
Nani tapewa likizo, WAGUMU twaulizana,
Leo ni kielelezo, siri itajulikana,
Penye wengi pana mambo.

Mboji mpenda kimwana, Ua akamletea,
Njiani akamwona, Joti memkumbatia,
Kajiumbua kimwana, bwenini kajifungia,
Penye wengi pana mambo.

Gati atia huruma, wamwona kama makapi,
Alidhani lelemama, kuwafanya wao pipi,
Waswahili walisema, njia ya mwongo ni fupi!,
Penye wengi pana mambo.

Hawa vidume wawili, hawakukata tamaa,
Wakabadili kauli, penzi wakalifufua,
Mtoto kawakubali, WAGUMU tukaduwaa!
Penye wengi pana mambo.

Nazo siku zikaenda, twaelekea hitimu,
Wakaanza kujiwinda, kwa nafasi ya kudumu,
Kimwana wakamganda, sawa na wendawazimu,
Penye wengi pana mambo.

Yakafika mahafali, nani atavishwa taji?
Gati kajificha mbali, katika pembe ya mji,
Ni Joti mara ya pili, kumzidi Kete Mboji!,
Penye wengi pana mambo.

Jambo likazua mambo, Mboji anaweweseka,
Mwenzetu kakosa pambo, japo alighalimika,
Gati kategua fumbo, kwa Joti amezimika!.,
Penye wengi pana mambo.

Mwisho Mboji kasadiki, kweli penzi siyo pesa,
Mtoto hakamatiki, hatimaye kamkosa,
Sasa imekuwa chuki, Gati pesa katakasa,
Penye wengi pana mambo.

Twashukuru mtihani, kwa kumaliza mzozo,
Yao macho vitabuni, wakasitisha mchezo,
Wote ‘bize’ masomoni, mtihani ndo kigezo,
Penye wengi pana mambo.

Tukahitimu cha sita, sote tukatawanyika,
Penzi lapata utata, mme mwenza karidhika,
Joti naye anasota, Gati ameshatoweka,
Penye wengi pana mambo.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment