For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Saa


Saa rangi yako nyeusi,
Ngozi yangu mnarandana,
Hukuundwa kwa almasi,
Bali umejengwa kwa nta,
Mlio wako maridhawa,
Damu yangu mmepatana,
Nikwonapo wanikonyeza,
Kisha waniambia muda.

Usiku ninaposinzia,
Waendelea kuzunguka,
Wasaa unapowadia,
Wanitekenya masikio,
Heshima unanitunzia,
Nisichelewe ofisini,
Betri nakuzawadia,
Kwa mwenendo wako mzuri.

Saa tuwapo matembezini,
Hakika ninajiamini,
Rafiki uliye mkweli,
Kila ninapokuhitaji,
Nikuvaapo mkononi,
Rohoni nahisi faraja,
Tuko sote kila mahali,
Wachangia mfanikio

Mwenzio ninakuhusudu,
Ni mengi umenitendea,
Unaniamsha kitandani,
Shughuli kuzipangilia,
Muda unaponitajia,
Ninajibidisha zaidi,
Sitokuachia daima,
Popote tutaambatana.

Saa unanitaarifu,
Shughuli za kutwa zatosha,
Ninapowasili nyumbani,
Ukutani umening’inia,
Umbile lako mduara,
Tik-tok wajizungusha,
Nami macho nakutupia,
Nikiwaza yaliyopita.

Mara waipiga alamu,
Kuna jambo wanikumbusha,
Nakujibu kwa tabasamu,
Mezani nikijisogeza,
Kuchovya inanilazimu,
Pasipo kufanya ajizi,
Kweli saa unanijali,
Ingawa umenigharimu!

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

Ujana


Hebu tazama jongoo, mwendo wake taratibu,
Siyo sawa na jogoo, asiye mstarabu,
Ang’aa kama kioo, hujikunja kwa adabu,
Ujana maji ya moto, jiulize mara mbili.

Vijana muwe makini, mngali bado na nguvu,
Kwa wazazi majumbani, kuweni wanyenyekevu,
Mwendo wa purukushani, wafaa mnyama ndovu,
Ujana maji ya Moto, tafakari kila Mara.

Masumbuko kuyashinda, ni kukwepa chokochoko,
Kila unachokitenda, kumbuka kule uliko,
Wapi unakoenda, na ni wapi utokako!,
Ujana maji ya Moto, tafakari kila Mara.

Unapokuwa kijana, damu bado yachemka,
Ni bora kukumbushana, katika kuwajibika,
Matumizi kuyabana, ili kutoaibika,
Ujana maji ya Moto, tafakari kila Mara.

Kujibidisha kazini, ndilo jambo la thamani,
Ugoigoi kichwani, wakusogeza shidani,
Maisha ya uzeeni, yandaliwa ujanani,
Ujana maji ya moto, baadae yatapoa
Miigo ya tamaduni, mfano ya Uzunguni,
Zafanya muwe njozini, kuishi ughaibuni,
Mwarejea utumwani, bila pingu mikononi!,
Ujana maji ya moto, kaa chonjo ujanani.

Wengi wanajikondesha, nakujikoboa sura,
Hakika wanachekesha, madoa sawa na vyura,
Weusi mnajishusha, kwani weupe ni bora?!,
Ujana maji ya moto, kaa chonjo ujanani.

Mitindo mwapendelea, isiyokuwa na radhi,
Mila kuzitupilia, mwajipunguzia hadhi,
Nasaha mwamomonyoa, kijadi mwatubugudhi,
Ujana maji ya moto, kaa chonjo ujanani.

Wapo wanyanyua vyuma, miili kupendezesha,
Migongo inawauma, vifua wavitunisha,
Kitabibu siyo vyema, mnapaswa kusitisha,
Ujana maji ya moto, kaa chonjo ujanani.

Wenye mikono mirefu, mwajitia kitanzini,
Jiepushe maradufu, kutupwa minyororoni,
Jengeni uaminifu, mfaidi uzeeni,
Ujana maji ya moto, kaa chonjo ujanani.

Katika hii sayari, walowengi wasumbufu,
Vipaji vyenu johari, mkuze kwa ubunifu,
Ni vyema mjiajiri, ajira zipo pungufu,
Ujana maji ya moto, kaa chonjo ujanani.

Ziongezeni juhudi, mkafaidi lenu jasho,
Utu na haki zaidi, uzeeni ukumbusho,
Kutii hamna budi, ninyi taifa la kesho,
Ujana maji ya moto, fainali uzeeni.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS