Ngoja nianze kwa kisa, kilichonifika mie,
Ni washuleni mkasa, ngoja niwasimlie,
Najua mnahamasa, naomba msisinzie,
Pole nitao wagusa, tena mnivumilie
Kwanza tukubaliane, ni Ukweli na Uwazi
Kokoriko! Naamka, nawaza kwenda shuleni,
Kwa-kwa! Shule nimefika, ngo-ngo! Wote paredini,
“mbona wewe unacheka, hebu lala sakafuni”,
Mwili wanisisimka, napo chapwa matakoni,
Kha! Maisha ya shuleni, kweli ni safari ndefu.
Mara vipindi vyaanza, wanafunzi twashtuka,
Hesabu ndicho cha kwanza, wengi tunahuzunika,
Kabla hatujaanza, bongo zaanza chemka,
Huyu bwana aongoza, kwa viboko kutunyuka,
Hii adhabu ni mbaya, yatutia wasiwasi.
Mwalimu anaingia, fimbo tatu mkononi,
Gafla namchukia, sielewi ni kwanini?,
Labda alichangia, hesabu kutotamani,
Nashindwa kuvumilia, najisikia huzuni,
Hii adhabu si nzuri, yatuvunjia heshima.
Kila siku atuchapa, hesabu kafanya chambo,
Tumwonapo twaogopa, apitako ana fimbo,
Ofisini ajitapa, wote wafate mkumbo,
Katunoa kama tupa, kwa kuyatunga mafumbo
Wengi wamesusa somo, kwa sababu ya viboko.
Leo ametoa swali, na mfano hakutoa,
Wote tumekosa swali, mfanoe hajatoa,
Mara! Fimbo mbilimbili, wote katuzawadia,
Nimefikiria mbali, kwa somo kutolijua,
Wengi wamesusa shule, kwa sababu ya viboko.
Kutoka katika kisa, mengi tumefundishana,
Niliyoeleza hasa, wengi mlishayaona,
Basi tuvipinge sasa, twepushe kudhuriana,
Tusiingize siasa, tukaja laumiana,
Fimbo sumu ya elimu, yapaswa kutokomezwa.
Wote walo watukutu, tiba yao si viboko,
Tawatia ukurutu, mithili ya mbwa koko,
Lakini watadhubutu, baada ya michubuko,
Jamani tujali utu, viboko siyo zindiko,
Fimbo sumu ya elimu, yapaswa kutokomezwa.
Weupe walianzisha, haki zetu kuzibana,
Kwanini tunajishusha, kwa fimbo twaumizana,
Mwendo huu tumekwisha, hatuwezi kufichana,
Mwenzenu zilinichosha, na sitaki kuziona,
Lo! Adhabu ya Viboko, Kasumba ya Kikoloni.
Watoto haki wapeni, tena kwa moyo mweupe,
Hata huko majumbani, viboko tusiwachape,
Wazazi tekelezeni, msifanye waogope,
Walimu tufatieni, zetu fimbo tuzitupe,
Lo! Adhabu ya Viboko, Kasumba ya Kikoloni.