For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Mwanga (Sehemu ya Pili)


Elimu sawa na Mwanga, ujinga ni kama giza,
Giza linatangatanga, ili mwanga kuumeza,
Vitabu ndiyo uganga, giza vinatokomeza,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Adui yetu ujinga, kazidi kuchachamaa,
Akili katia chenga, mkaa kaipakaa,
Vichwani kuna mchanga, ubongo umechakaa,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Gizani siyo patamu, patufanya tusumbuke,
Mwanga ushike hatamu, kwa wanaume na wake,
Mshike sana elimu, simwache aende zake,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Wananchi mtambue, hili nalowakumbusha,
Giza lisiwakomoe, tamaa kuwakatisha,
Jamii ijikomboe, elimu mwanga wa maisha,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Penye kutetea haki, elimu ni ufunguo,
Bila hata kuhamaki, waweza mipangilio,
Nyuma nyuma hutobaki, kwako mbele ni chaguo,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Wafanyie tathimini, waliopita shuleni,
Mawazo yao makini, tena wanajiamini,
Tazama wanazuoni, mwenyewe utatamani,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Tuliweka azimio, hafe adui ujinga,
Hataki maendeleo, kila mara atupinga,
Simpe upendeleo, mbele twataka kusonga,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Taasisi za elimu, zipo nyingi duniani,
Kusoma iwe muhimu, ili tutoke gizani,
Tuonesheni nidhamu, na bidii mafunzoni,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Tuboreshe mazingira, Taasisi za Elimu,
Tusome bila harara, kuyamudu majukumu,
Elimu iliyobora, kujali ubinadamu,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Mkiwa wataalamu, mwajibike bila mbwembwe,
Japo mapato hadimu, shughuli zitekelezwe,
Nasi wadau wa elimu, tujifungeni vibwebwe,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Tuzidi kuhimizana, ujinga tutokomeze,
Masomo kukumbushna, na mafunzo tumalize,
Elimu mwisho haina, sote tujiendeleze,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Sehemu za kusomea, nazo zikidhi ubora,
Vitendea kazi pia, vyendane na mazingira,
Ujinga kutokomea, tuboreshe mishahara,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment