For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Mama Zetu (Sehemu ya Kwanza)


Toka mwanzo wa dunia, mwawaona watu duni,
Ni wachache twajutia, japo hatuna idhini,
Nao wazidi umia, haki zao mashakani,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi

Hasa huku Afrika, mfumo dume wazidi,
Mila zetu zasifika, wa kike kuwakaidi,
Sijui yetu hulka, kubinya ua waridi!,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Wengi wanalazimishwa, ndoa na wasiorika,
Babu zao waodheshwa, bila wao kuridhika,
Kweli mnataabishwa, ni lini mtaboreka?
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Kwa upande wa elimu, hawana kipaumbele,
Wa kike mwawadhurumu, ili wasisonge mbele,
Kusoma sasa muhimu, tuachane na ukale,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Wajane waliofiwa, wanyang’anywa mali yote,
Watakiwa kurithiwa, na shemejiye yeyote,
Lini watathaminiwa, moyoni wametemete?
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Ugawanaji mirathi, kimila tunawatenga,
Na tena wapo baadhi, wafukuzwa kwa mapanga,
Kisheria wana hadhi, japo mwawapiga chenga,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Wapo mnaowaita, eti mama wa nyumbani,
Wapigwa kila nukta, kama mdundo ngomani,
Tena bila ya kusita, mateke hadi tumboni,
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

Kwenye soko la ajira, twawabagua kwanini?
Kuwajiri ni nadra, wapewa vyeo vya chini!,
Twasababisha harara, mwenendo tuupingeni,
Hawa ndio mama zetu, mnanitia uchungu!.

Kila tunachokiweza, wao pia wanaweza,
Mbona tunawadumaza, hebu jaribu kuwaza,
Wajuzi twawapoteza, ndilo linaloshangaza.
Hawa ndio mama zetu, yatubidi tuwaenzi.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment