For Proofreading, Copy-editing, Substantive Editing of Research or Conference Papers, Reports, Manuscripts, Thesis; call: +255 716 23 1772 or E-mail: jaba@udsm.ac.tz

Mwanga (Sehemu ya Kwanza)


Kuna giza mbele yangu, japo mie si kipofu,
Nyuma naona ukungu, ninakoenda sihofu,
Japo naonja vichungu, moyo wangu mkunjufu,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Mwendo mithili ya kaa, upande nachechemea,
Gafla ninajikwaa, nanguka kama gunia,
Ubongo umedumaa, giza limeninamia,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Usiku umeingia, njiani ninatembea,
Giza linavizia, nyota zinanizomea,
Mwezi waniangazia, ninazidi kujongea,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Tupo tulio shimoni, hatuoni pa kushika,
Tunapapasa gizani, nuru imeshatoweka,
Yowe twatoa kinywani, ni mwangwi tu wasikika,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

Gizani kuna vitisho, vyatufanya tuogope,
Tufanye matayarisho, kabla ya kuja kupe,
Mwanga usiwe na mwisho, na sote tuwe peupe,
Mwanga wafukuza giza, kutogubika dunia.

  • Digg
  • Del.icio.us
  • StumbleUpon
  • Reddit
  • RSS

0 comments:

Post a Comment